Maswali kuhusu wito wa kuwa Sista wa MM

Maswali yenu yamejibiwa

Kama uko na swali kuhusu wito katika shirika la MMM tafadhali wasiliana nasi na utapata jawabu yako binafsi.

Anna anauliza...

Kuna tofauti gani kati ya maisha ya kuwa sista wa MMM na kufanya kazi ya kujitolea au kuwa daktari mlei katika nchi zinazoendelea kukua ama mfanyakazi katika shirika lisilo la Kiserikali?

aeriel_view_of_chiulo_crop1Anna, mara nyingi tunaulizwa swali hili hili! Sista wa MMM anajitolea maisha yake yote kuishi katika jumuiya ya masista na kutumia talanta zake kufanya kazi anapotakikana. Kama Abrahamu, anasikia Mungu akimuita "Acha nchi yako na uende mpaka nchi nitakayokuonyesha".  Wanaojitolea bila kuwa watawa ni muhimu sana, ila lazima mtu ajikaze mhanga. Masista wanaenda kwa watu fulani, wanaishi nao, na wanawasaidia kujitegemea wakati wanapoishi nao mpaka wakati ambapo huduma zao hazihitajiki tena.

Anna anataka kujua zaidi...

Je, sista anaishi katika nchi moja maisha yake yote?

archbold-c2Inategemea, Anna. Baadhi ya masista wameishi katika nchi moja karne nyingi, wanarudi tu nchini mwao baada ya miaka miwili au mitatu kwa likizo. Walakini, kulingana na mabadiliko ya maisha na hitaji ya shirika, masista wanaweza kutumwa tena katika nchi mpya (tofauti). Kuaga jumuiya moja na kujiunga na jumuiya nyingine mpya sio jambo rahisi. Kujiunga na jumuiya mpya pia kunachukua muda. Kunahitaji usaidizi na uhimizaji kustahimili mabadiliko katika maisha kwa watu wote, sio masista tu! Katika hii picha, unamuona Sista Brigid Archbold mwenyeji wa Ireland ambaye ameishi nchini Angola kwa muda wa miaka 45 na hangependa kuhamia sehemu ingine yeyote!

Lucia anaulizia kuhusu maisha ya kiroho...

Ni kwa njia gani maisha ya kiroho yanasaidia MMMs kufanya kazi wanazofanya?

prayer-crop2Asante kwa kuuliza hili swali, Lucia! Kujitolea kwetu ni kwa Kristu anayeita kila mmoja wa masista kufuata wito wake. Wito wa Kristo ndio nguvu yetu ya kuendela mbele. Wakati tukijitolea kutumikia watu katika mambo ya afya, tunachukua muda kila siku kusali, sala za mtu binafsi na za jumuiya. Nikatika ukimya wa sala zetu tunapata nguvu za kuendelea na wito wetu hasa kupata salama katika hali ambazo pengine zinadai nguvu zaidi na pia sehemu ambazo hazina usalama.

Nadia anataka kujua namna siku katika utawa inavyokuwa ...

Siku inakuwaje katika maisha ya utawa?

sunset_angola_smallHabari Nadia, nivigumu kuelezea kwa kifupi jinsi siku katika usista inavyokuwa, kwa sababu siku zinatofautiana sana! Katika Afrika na Amerika ya Kirumi siku huanza mapema sana. Saa ya kuamka hutegemea ratiba ya misa katika sehemu ambazo masista wanafanya kazi. Inaweza kuwa saa kumi na mbili asubuhi ama mapema zaidi. Baada ya kifungua kimya kila mtu huharakisha kwenda kazini au shuleni. Katika nchi za magharibi, siku huanza baadaye kidogo, isipokuwa wakati sista anaharakisha kukwepa msongamano wa magari au anaelekea katika uwanja wa ndege kwa safari ya mapema. Katika Afrika, ni kawaida kupumzika kidogo baada ya chakula cha mchana, wakati jua liko kichwani, na baadaye kuendelea na kazi jua likipungua. Baada ya shughuli za mchana, jioni tunajumuika wote kwa sala za jioni hasa kwa wale wanaoweza kuhudhuria. Kuandaa sala za jioni kunaweza kuwa kazi ya ubunifu mkubwa, hasa wakati kuna masista wa umri mdogo ambao wanaweza kucheza gitaa, ngoma na vyombo vingine vya mziki. Wakati wa sherehe muhimu, kunaweza kuwepo kucheza na ishara nyinginezo za kiliturgia. Kwa kawaida, huwa tunaimba zaburi, ama zinaweza kuwa sala za kimwa kimwa katika jumuiya zenye masista ambao wamezeeka.

Raquel angependa kujua kuhusu vipaji vya mtu binafsi...

Je masista wanafanya mambo ya kibinafsi ya kujifurahisha au kukuza vipaji vyao kando ya kazi na sala?

birds-crop1Ndio Raquel, kwa kweli tunafanya mambo ya kujifurahisha wakati hatuko kazini. Kwa hakika, kila sista anahimizwa kuwa na jambo ambalo anaweza kujishughulisha nalo wakati hayuko kazini. Utapata masista wengi wanajihusisha na mambo ya kisanaa na ufundi wa namna nyingi. Wengini wanapendelea kazi ya upigaji picha - na ndio maana tuko na picha nyingi sana katika mtandao wetu! Wengine ni maarufu kwa upangaji wa maua. Wengine wanapenda muziki - wale ambao wanajua mziki na wanaweza kupiga chombo chochote cha muziki wanadhamana kuu katika jumuiya. Kuna sehemu nyingi za kukuza vipaji vya masista wetu pamoja na kazi yetu wa matibabu. Sista Marian Scena, kutoka USA ni daktari mwenye kazi nyingi sana huko Tanzania. Ni mmoja wa wale ambao wamekubuhu katika sanaa ya utazamaji wa ndege. Anaandika kuhusu 'Jinsi shughuli zangu za kujifurahisha zinavyosaidia kazi yangu ya kitaalamu'

Elizabeti anasema  hajaelewa vizuri kazi haswa ambazo MMM wanafanya ...

Kazi haswa ya MMM ni gani? Sijaelewa vizuri.

nigeria_gusorro_felicitas5_smHili sio jambo la kushangaza, Elizabeti, kwasababu kuna kazi nyingi katika wito wa MMM na utume wao. Ukitembelea tofuti yetu, nchi baada ya nchi utaona jinsi kazi zetu ni za namna nyingi kulingana na mahitaji ya sehemu tunazofanya kazi. Utunzaji wa afya hasa afya ya kinamama na watoto wao inapewa kipaumbele katika kazi za MMM. Hii inamaanisha kufanya kazi hospitalini ama katika zahanati, lakini inaweza pia kuwa katika parokia - kama ilivyo kule Brazil na Honduras. Ukitoka katika mambo ya afya, masista wengi wanahusika katika mambo ya utawala katika ngazi tofauti. Wakati tunapoenda katika sehemu mpya, tunawasikiliza wenyeji wakitueleza mahitaji yao na tunawahusisha katika kazi ya utafiti kubuni jinsi ya kufuata kukidhi mahitaji yao. Sheria yetu ni kwenda sehemu zile ambazo watu wana mahitaji zaidi ya lazima na kujaribu kusaidia pale ambapo serikali au Mashirika yasiyo ya kiserikali hawajaweza kutekeleza. Tunajaribu kuwa wabunifu ipasavyo. Hio inamaanisha kwamba mara nyingi tunaenda sehemu au kufanya kazi ambazo hazituletei sifa au fahari! Picha yetu inaonyesha Sista wa MMM kutoka Nigeria, Sista Felicitas, ambaye aliitwa machweo (jua linapotua) kutembelea familia moja ambayo mtoto alizaliwa katika sehemu za mashambani kaskazini mwa Nigeria. Baada ya kuhudumia mtoto mchanga na mama yake, watu wengine wengi sana walimletea watoto wengine waliokuwa na magonjwa tofauti kutafuta ushauri wake.

Kate anaulizia kuhusu masomo ya kitaaluma ...

Je, ni lazima niwe nimesomea taaluma ya udaktari au uuguzi kabla ya kujiunga na MMM? Je inategemea kazi ambayo nimesomea ama shahada au vyeti vya elimu nilivyonavyo?

aror_bridie_sick_child_sm2La, Kate, sio lazima kuwa umesomea kazi fulani kabla ya kujiunga na MMM. Unahitaji kuwa umepita vizuri mtihani wa mwisho wa sekondari katika nchi yako. Isipokuwa, wengi wanojiunga na shirika la MMM tayari wameshafanya kazi tofauti kwa miaka kadhaa. Umri wa wastani wa wale ambao wanajiunga nasi ni kama 25 au 26, lakini wengine wana umri mdogo au zaidi kushinda huu wa wastani. Wengi wanaojiunga na MMM wanakuwa na elimu msingi katika mambo ya kiafya, wachache wamehitimu zaidi katika kazi hii. Pia tuna wanawake ambao wanajiunga na vyeti vya biashara na mambo ya uenezaji wa habari, upishi, sociologia, ualimu, teologia nk. Kuna kazi kwa wote katika MMM! Sista Bridie Canavan, anayeonekana katika hii picha, alijiunga na novisiati ya MMM nchini Ireland, baada ya kuweka nadhiri zake za kwanza alisomea uuguzaji na ukunga. Hii picha ilichukuliwa nchini Kenya, ambako wagonjwa hupendelea kulala chini ya kivuli wakati wa mchana na kuingia ndani tu jioni.

 

Christina anaulizia kuhusu nadhiri za utawa

Ni nadhiri gani ambazo masista wanaweka? Kutooa au kutokuwa na mali binafsi kuna faida gani?

uganda_kitovu_maura_lynch_operating_smHili ni swali muhimu sana Christina! Katika maisha ya kawaida ya utu-uzima, mtu anakuwa na uhuru wa kuchagua mahali pa kwenda au ninani anaishi naye, pia unaweza kuzuiliwa kufanya mambo haya kwa sababu ya majukumu katika familia. Kwa kuchukua nadhiri za useja, umaskini na utiifu, sista anakuwa tayari kwenda kutumikia popote anapohitajika. Hapaswi kuwa na mali nyingi ya binafsi ili aweze kusafiri kwa haraka popote kuitikia wito wake, akitegemea hela kidogo ya matumizi binafsi. Sista Maura Lynch, anayeonekana katika hii picha ni daktari wa upasuaji ambaye amefanya kazi nchini Angola na hivi juzi kule Uganda. Sista Maura angekuwa anafanya hii kazi kwa manufaa yake binafsi, wale ambao amekuwa akiwatumikia wasingeweza kulipa malipo ya upasuaji. Badala yake amechukua changamoto ya kuanzisha kitengo cha upasuaji wa 'obstetric fistula' shida ambayo inawapata kina mama wengi sehemu nyingi za bara la Afrika. Sista Maura amejitolea kabisa kusaidia kina mama ambao wako na shida hii na kwa hivyo hatafuti mali yake binafsi!

Renata anaulizia kuhusu maisha katika jumuiya...

Jumuiya inategemea majukumu gani kutoka kwa masista? Ni nini manufaa ya kuishi katika jumuiya? Ni usaidizi gani unaopata kwa kuishi katika jumuiya?

felicia_muoneke_anastasia_essien_crop_smallMaisha katika jumuiya ya MMM ni kama maisha katika familia. Sista anaishi katika jumuiya kama katika familia, ambapo kuna kuishi pamoja, kusaidiana na kujipumzisha. Haya yote hupatikana kwa kuwepo kutumikia wengine, kuomba pamoja na kukaribisha wote wanaotembelea jumuiya. Masista wote wanatumia kwa pamoja mishahara na mali nyingine yeyote ambayo wanapata. Mahitaji ya kila mtu katika jumuiya yanaheshimiwa. Hii inahitaji moyo mkarimu wa kutoa na kupokea. Hawa masista wanaonekana katika hii picha wanatoka Nigeria. Sista Felicia (kushoto) ni daktari na Sista Anastasia ni Msimamizi. Kazi tofauti wanazofanya masista zinasaidia kuboresha maisha katika jumuiya.

Renata ana swali lingine...

Je, ni vigumu kuishi katika jumuiya?

nigeria_christine_gill_smJibu ni ndio au la, Renata. Maisha katika jumuiya kama maisha yeyote yana mazuri na mabaya yake. Uzuri wa kuishi katika jumuiya ni kwamba kunakuwa na ushirikiano mwema na kuelewana pamoja na kuwa na lengo moja. Anakuwepo mtu wa kusaidia wakati maisha yanakuwa magumu. Tunajaribu kuishi katika jumuiya zilizochanganyika tamaduni tofauti. Hii inasaidia sana - lakini inamaanisha pia kuwa tayari kusoma vitu ambavyo ni vya dhamani katika tamaduni nyingine, aina ya vyakula na muziki, nk. Vivyo hivyo, hii inahitaji kusikiliza kwa utulivu na kukubali tofauti kati ya tamaduni, na kuwa na moyo wa kutoka katika 'mambo ambayo umezoea katika utamaduni wako' na kwenda  zaidi ya hayo na kufikiria zaidi kupokea mambo ambayo ni muhimu katika maisha ya wengine. Masista wa MMM wanafuata sheria ya Mtakatifu Benedikto ambayo inakubali utofauti. Kwa mfano, anasema kwamba wakati wa chakula, aina mbili za chakula ziwepo ili wale ambao hawawezi kula mojawapo ya chakula kimoja, wanaweza kula kingine - kuonyesha heshima kwa wale ambao ni tofauti. Katika hii picha unaona Sista Christine Gill, iliyochukuliwa huko Nigeria alipokuwa akijiandaa kwenda 'mobile clinic' katika jamii moja ya wafungaji inayoitwa Fulani. Akirudi jioni, atafurahi sana kuwa nyumbani aoge na maji yaliyopaswa joto na sola. Baada ya sala za jioni, wakati wakila chakula cha jioni, wanajumuiya ambao ni watatu au wanne wanazungumzia waliyoyafanya na kushuhudia siku yote, iwe ni magumu, mazuri, au mapya.

Natalia anataka kujua kwa nini masista wengine wanavaa kitambaa cha usista kichwani...

Katika nchi yangu ya Poland, kuna mashirika ambayo masista wao wanavaa kitambaa kichwani na wengine hawavai. Ni wazi, njia moja au nyingine. Kutoka kwa tofuti yenu inaonekana kwamba masista wengine huvaa na wengine hawavai. Je unaweza kuelezea tofauti?

florence-gladys-smallVizuri, Natalia, zamani kila Sista alivaa kitambaa kichwani, ila siku hizi kuna uhuru wa kuvaa au kutovaa. Kila Sista anaamua mwenyewe. Isipokuwa, tunaangalia pia mategemeo ya watu tunaotumikia na pale tunapopaswa kuvaa kitambaa, tunavaa tukiwa kazini na wakati tunatoka nje. Wakati wa shughuli rasmi tunavaa nguo ya rangi ya urujuani, sio sare rasmi. Katika Afrika hii inaweza kuwa nyeupe yote. Tunavaa pia mfano wa Kutembelewa kwa Elizabeti na Bikira Maria wakati alipokuwa mjamzito. Hii inaweza kutengenezwa na shaba au kutengenezwa kutoka kwa maganda ya nazi. Kila sista hupata pete ya dhahabu wakati anapoweka nadhiri zake za daima. Isipokuwa, katika nchi zingine, hasa Amerika ya Kirumi, masista hupendelea kuvaa pete nyeusi ambayo ni ishara ya kujitolea kwa maskini na mazingira yao. Je, swali lako limejibiwa?

Sandra anataka kujua nani anaenda wapi ...

Je Sista anaweza kuchangua (anakuwa na usemi kuhusu) nchi anayoenda kufanya kazi?

malawi_dumka_improved_latrine_sm1Ndio, Sandra, anakuwa na usemi, ila hawezi kujiamulia mwenyewe. Kiini muhimu katika maisha ya MMM ni kujitolea kwa Mungu na kuwepo kutumikia watu wa Mungu mahali ambapo unahitajika zaidi. Ila, kunakuwepo mazungumzo hili kuhakikisha kwamba sista anafurahia na ako tayari kujitolea hata wakati haridhiki! Wengi wetu tunashangaa sana jinsi mafanikio hupatikana mwishoni. Sista Dumka Michael, anayeonekana katika hii picha anasema kwamba hakuwa na sehemu aliyopendelea kufanya kazi kwa sababu alijua tu nchi yake ya kuzaliwa ya Nigeria na nchi ya Kenya ambapo alifanyia masomo yake ya usimamizi. Mpaka sasa, amefanya kazi Malawi miaka kadhaa na anapenda Malawi sana. Katika hii picha, anajaribu mtambo mdogo wa kunawia mikono nje ya nyumba moja.

Petronilla anaulizia kuhusu mambo ya afya binafsi...

Je, afya yangu inaweza kunizuia kujiunga na MMM?

motherhouse_2007Kama unavyoona katika tofuti yetu, Petronilla, maisha ya utawa na umisionari yana kazi nyingi. Kwa hivyo, afya nzuri ya kimwili na akili inatakiwa kwa wale ambao wanataka kujiunga na MMM. Afya ya mtu binafsi ni baadhi ya vitu ambavyo huangaliwa katika novisiati na miaka ya kwanza ya malezi. Baada ya kuweka nadhiri, hakuna mtu ambaye anaombwa kuondoka shirika kwa sababu ya hali yake ya kiafya. Wakati mmoja au mwingine huwa tunaugua magonjwa tofauti na masista wetu wagonjwa na wazee wanachangia zaidi katika maisha ya sala. Hii picha inaonyesha nyumba yetu ya kwanza nchini Ireland ambapo masista wengi ambao wamestaafu wanaombea kazi zetu pamoja na wale ambao wanatusaidia kutekeleza kazi zetu duniani kote.

Maria anawaza kuhusu mawasiliano na familia yake...

Ni mara ngapi Sista anaruhusiwa kukutana na familia yake?

malawi_hbc_volunteers2_smInategemea, Maria, kulingana na hali. Wakati wa Novisiati, masista hawaruhusiwi kutoka nchini, ila kama kuna msiba nyumbani, wanaruhusiwa. Wakiwa kazini ngambo, wanapata likizo ya miezi mitatu baada ya kila miaka mitatu, sehemu ya hii miezi mitatu huruhusiwa kutembelea familia. Katika nchi ambazo hali ya hewa si nzuri sana au ni ngumu kufanya kazi, likizo inakuwa kila miaka miwili na huwa ya miezi miwili. Mara nyingi, sherehe ya kuweka nadhiri za mwisho hufanyika katika parokia ya nyumbani ya sista mhusika. Sista Cecily Bourdillon, aliye katika hii picha, ni daktari ambaye anasimamia kazi ya matibabu kule Chipini nchini Malawi. Ni mzaliwa wa Zimbabwe, lakini familia yake wanaishi katika nchi tofauti kwa hivyo hawezi kuwaona mara kwa mara. Ila, ni mmoja wa masista wa kwanza kutumia barua pepe, mwanzoni mwa mwaka wa 1990! Sasa, kwa sababu ya barua pepe, amepata nafuu ya kuwasiliana na familia yake.

Nilza anashangaa kuhusu swala la lugha...

Je, ni lugha gani zinazohitajika? Ni lazima mtu aweze kuzungumza kingereza mwafaka? Ni lugha gani masista wanatumia kuwasiliana na watu ambao wanaishi nao?

malawi_kasina7b_sm1Hili ni swala nyeti, Nilza! Lugha ya kufanya kazi katika shirika ni kiingereza. Baadhi ya kina mama hujiunga na shirika la MMM bila ufahamu wa kutosha wa lugha ya kiingereza na wanafundishwa kuzungumza lugha vizuri kabla ya kujiunga na novisiati. Ni wazi kwamba kuishi katika jumuiya ambayo kiingereza hutumika kama lugha ya kila siku kunasaidia kuelewa lugha vizuri. Lugha nyingine ambazo hutumiwa ni kama Kiswahili, Kifaransa, Kispanish, na Kiportuguese. Masista hujitahidi kama wamisionari kuelewa lugha ya taifa katika nchi ile wanayofanyia kazi. Masista wengine pia wamejifunza baadhi ya lugha za makabila mbalimbali katika Afrika pamoja na lugha ya taifa. Katika sehemu nyingine, kuna uwezekano wa kufanya kazi kupitia mkalimani. Katika hii picha, Sista Clara (anayeketi) ni mzaliwa wa Malawi. Kwa sababu anaelewa lugha na utamaduni wa hii nchi, Clara ni wa dhamani kubwa sana katika kazi zetu katika zahanati ya Kasina. Vinginevyo, sista Mary McNamara (anayesimama) angehitaji mkalimani.

Joan ana swali kuhusu jinsi ambavyo pesa za kuendesha kazi za masista wa MMM hupatikana...

Masista hupata kutoka wapi hela za kazi zao?

kathie_shea_child_2008Mkuu wa kazi za shirika pamoja na uongozi mkuu katika shirika wana wajibu wa kuhakikisha kwamba kuna pesa za kutosha kutekeleza miradi ya masista pamoja na kuhakikisha kwamba maelezo kuhusu matumizi ya hizo pesa yanatolewa kwa njia ifaayo. Mishahara wanaopata masista pia hutumika na masista wote kwa jumla, kila sista huwa anapata hela ya mfuko inayotolewa kulingana na hela ya nchi ambayo hufanya kazi. Shirika pia hulipia nauli na mahitaji mengine yanayo wawezesha masista kutekeleza kazi yao ya kuhudumia wagonjwa. Anayeonekana katika picha hii ni Sista Kathie Shea kutoka Amerikani ambaye anatishahada ya kusimamia biashara. Anaishi huko Nairobi lakini hutembelea nchi nyingi kusaidia masista na mambo ya fedha. Masista ambao wanasimamia kazi zetu huwakilisha maombi ya msaada kwa wafadhili tofauti. Tuna watu ambao pia hufanya kazi na MMM kuchangisha pesa za kuendeleza kazi zetu. Tunashukuru siku zote kupokea msaada, ijapokuwa kidogo, kutoka kwa watu binafsi wanao na nia ya kusaidia kazi zetu. Msaada kupitia tofuti pia ni muhimu sana kwetu. Yeyote anaweza kutoa msaada sasa! (Donate Online).

Karina anaulizia kuhusu kazi za maendeleo ...

Pamoja na huduma za matibabu, nikiangalia tofuti yenu, nafikiria baadhi ya Masista wa MMM wanahusika sana na kazi za maendeleo. Je, ni ukweli?

hannelly_smNdio kabisa, Karina. Sehemu haswa za kazi za maendeleo ni kuhusu maendeleo ya wanawake, kazi za kuleta mapato, miradi ya maji safi na chakula bora. Hutoaji wa maji safi ni mhilimili katika kazi zetu. Kwa kweli, masista hawachimbi visima vya maji wenyewe, lakini wanafanya kazi na maofisa wa serikali na hasa kuwahamasisha watu kuungana na kupanga uchimbaji wa maji pamoja na utuzaji. Masista wengi wanafahamu sana namna ya kutafuta pesa za uchimbaji pamoja na wachimbaji halisi. Sista Dympna Hannelly, anayeonekana katika hii picha akiwa Makondo nchini Uganda, ni mtaalamu katika mambo ya afya ya jamii.

Teresa anashangaa ni tofauti gani ambayo tunaweza kuleta wakati mahitaji ni mengi sana...

Inawezekanaje kuleta tofauti wakati kuna umaskini na ugonjwa mwingi katika nchi nyingi ambazo mnafanya kazi?

nkeiru_edochie_with_cabbageSawa sawa Teresa, ni ukweli kwamba umaskini umesambaa sana na hii ndio maana watu wengi wana afya mbaya. Ila, tunafikiria kwamba ingekuwa njia rahisi kusema hatuwezi kusaidia kwa vyovyote. Mambo mawili muhimu ambayo tunaweza kufanya ni kusaidia jumuiya kuangalia mambo ya chakula bora na maji safi. Picha iliyo hapo juu inaonyesha Sista Dympna ambaye amesaidia uchimbaji wa visima kadhaa vya maji nchini Uganda. Hapa, unaona picha ya Sista Nkeiru ambaye ambaye ni mwuguzaji na mkunga katika zahanati ya Zaffe Jahmuri ya Benin. Anadhamini sana shamba letu la maonyesho. Zahanati yetu hufanya kazi pamoja na wakulima hili kuboresha mbinu zao. MMM pia wanashirikiana kazi na Kituo cha Elimu ya Maendeleo cha Songhai.

Ciara anaulizia kuhusu msaada wa dharura...

Je, kuna tofauti kati ya kazi zenu na kazi za mashirika ya msaada wa dharura?

rwanda_kirambi_survey2Ndio Ciara, kuna tofauti kubwa! Sisi huenda kwa watu ambao wanatualika kuwasaidia hasa katika huduma za afya na tunaishi nao, na kuwafundisha yote tunayojua lakini tukiwa na matarajio ya kuhamia sehemu nyingine. Hio inaweza kuchukua miaka mingi! Wakati mwingine tumeenda kwa kazi ya dharura katika sehemu fulani na baada ya hio dharura tumebaki na watu muda mrefu baada ya dharura kuisha. Mfano mwema ni kama njaa kubwa iliyowapata watu katika jangwa la Turkana mnamo mwaka wa 1962. Tumeondoka katika hio kazi mwaka wa 2009 tu! Mfano mwingine ni Rwanda. Tulienda pale mara ya kwanza mwezi wa sita mwaka 1994 wakati wa mauaji ya umati na bado tuko huko. Picha yetu hapa inaonyesha Sista Helen Spragg, mtaalamu wa madawa kutoka Uingereza, akifanya uchunguzi wa kwanza nchini Rwanda baada ya vita kutulia kiasi. Mfano mwingine ni wa Honduras. Tulienda kule mwaka wa 1998 baada ya kibunga Mitch, na baadaye tukaanzisha vituo viwili ambavyo masista wa MMM bado wanaendelea kufanya kazi kati ya wahudumu wengine wa kiafya. Masista wengine wanaweza kuruhusiwa kwa muda mfupi kufanya kazi na mashirika ya dharura hasa wakati wa ukame au mkasa mwingine.

Kama uko na swali kuhusu wito katika shirika la MMM, tafadhali wasiliana nasi na utapata majibu yako binafsi.

Search...